Kutukana Viongozi Matusi ya Nguoni ni Utoto - Matusi Hayajengi Hoja.
- Rev. Godwin Chilewa
- Nov 22, 2024
- 3 min read

Katika jamii ya kisasa, kuna ongezeko la vijana ambao wanaotumia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya umma kutukana na kutoa lugha chafu kwa wanaharakati, viongozi wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na wanasiasa, wachechemuzi, viongozi wakuu wa serikali, na hata Rais wa Tanzania. Tabia hii imezidi kuota mapembe kwa kisingizio cha haki ya kusema (uhuru wa kujieleza) na demokrasia.
Mbaya zaidi ni kwamba jambo hili limeelekea kukubalika hata na viongozi wa chama tawala. Yapo makundi ya vijana wa UVCCM yanayoshinda mitandaoni kutukana viongozi wa upinzani na wanaharakati bila aibu, tena huku wakipeperusha bendera ya chama. Hata hivyo, tunapaswa kutambua kwamba kumtukana mtu yeyote, licha ya kiongozi wa kitaifa si tu kujitengenezea uadui dhidi ya mtu au kiongozi huyo, bali pia ni kinyume na mila na maadili ya Kiafrika, na pia ni kinyume na mafundisho ya dini. Uwe mwana CCM au shabiki wa chama cha upinzani, matusi hayawezi kukuinua, HAYAJENGI.
Niweke bayana hapa kwamba kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake, kumshauri kiongozi pale anapokosea, na kumkemea kama akifanya mambo ya hovyo, tena kwa nguvu zote. Lakini haya yanapaswa kufanyika kwa lugha ya kiungwana, isiyodharilisha utu wa mtu, wala kuchochea vita na kisasi. Hii ni kwa sababu kila mtu anastahili heshima na kuthaminiwa utu wake, na pia viongozi ni watu wenye familia zao. Si hivyo tu, bali pia ni vizuri kumtendea mwingine vile upendavyo kutendewa. Kwa ujumla matusi si lugha inayofaa kutumiwa na muungwana yeyote.
Katika tamaduni za Kiafrika, kuna methali nyingi zinazohimiza heshima kwa viongozi, mfano: “Mfalme ni mfalme kwa amri ya Mungu,” au “Mwenye nguo nzuri huonekana kama mfalme.” Methali hizi zinatufundisha kwamba kiongozi anapaswa kuheshimika si tu kwa nafasi aliyonayo, bali pia kwa wajibu wake wa kusimamia haki na amani katika jamii. Ni muhimu kumkosoa anapokosea lakini si kwa matusi ya nguoni kiasi cha kutweza utu wake. Kufanya hivyo kunaweza kuleta machafuko katika jamii.
Tena, Biblia inatufundisha kwa uwazi kuhusu heshima kwa viongozi na mamlaka waliyopewa. Katika Warumi 13:1-2, inasema: “Kila mtu na atii mamlaka iliyo juu yake; kwa maana hakuna mamlaka isiyokuwa kutoka kwa Mungu, na yaliyopo yote ni ya Mungu aliyekubali.” Hii inamaanisha kwamba viongozi ni sehemu ya mpango wa Mungu, na hivyo ni muhimu kuwa na heshima kwao. Katika Kutoka 20 Mungu anaonya akisema “Waheshimu baba yako na mama yako siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana Mungu wako. Ingawa hapa baba na mama huchukuliwa moja kwa moja kuwa wazazi, lakini hilo pia linaweza kuwa fumbo la kutukumbusha kuwaheshimu wale waliotutangulia au wanaotuzidi mamlaka.
Pia, katika 1 Timotheo 2:1-2, Paulo anasema: “Basi, naombeni dua kwa ajili ya wafalme na kwa ajili ya wote walioko katika nafasi za juu, ili tuishi kwa amani na utulivu katika utauwa na adili.” Hii ni ishara wazi ya kuwa ni wajibu wa kila Mkristo kuombea viongozi wao ili wawe na hekima ya kutawala, na pia kwamba tunapaswa kuwa na amani na heshima kwa viongozi wetu.
Hata katika Quran, kuna mafundisho yanayohimiza heshima kwa viongozi. Katika Surah An-Nisa (4:59), Allah anasema: “Enyi mliyoamini! Mtii Allah, mtii Mtume na mtii wale wenye mamlaka kati yenu…” Hii ni dalili kwamba waislamu wanapaswa kutii na kuheshimu viongozi wa jamii zao, kwani ni sehemu ya mpango wa ki-Mungu.
Tabia ya kutukana viongozi haileti faida kwa jamii yoyote. Badala yake, inaweza kuleta machafuko, mgawanyiko, na kupunguza imani . Pia inaweza kuvuruga utulivu wa taifa na kuhamasisha chuki na vurugu miongoni mwa watu. Hivyo, ni muhimu vijana watambue kwamba haki ya kusema na kutoa maoni haipaswi kugeuzwa kuwa haki ya kudhalilisha utu wa mtu. Kwa ujumla mabadiliko ya kijamii hayahitaji lugha chafu na dhihaka. Badala yake, changamoto na maoni yanapaswa kuonyeshwa kwa njia ya heshima, hekima, na kwa njia zinazohimiza majadiliano ya maana. Mjadala wa kisiasa na kijamii unapaswa kuwa na lengo la kuboresha jamii, si kuleta machafuko.
Hitimisho
Kutukana viongozi na viongozi wa taifa ni tabia inayoharibu na kudhoofisha jamii. Heshima kwa viongozi ni msingi wa amani, umoja, na maendeleo. Kulingana na mila za Kiafrika, mafundisho ya Biblia na Quran, ni muhimu kumheshimu kiongozi, kwani ni sehemu ya mpango wa Mungu na jamii. Hivyo, vijana wanapaswa kujitahidi kuonyesha heshima kwa viongozi wao na kuepuka matumizi ya lugha chafu, ili kujenga taifa imara, lenye amani na maendeleo.
Rev. Godwin Chilewa
Comments