Ubaguzi Katika Mfumo wa Demokrasia Tanzania - Nani Anapendezwa na Aibu Hii?
- Rev. Godwin Chilewa
- Nov 9, 2024
- 5 min read
Updated: Nov 10, 2024

Kwa miaka mingi Tanzania ilijijengea sifa ya kuwa nchi inayofuata misingi ya demokrasia na utawala bora. Tangu kupata uhuru wake Tanzania imekuwa haina shida katika taratibu za kubadilishana kiti cha urais na uongozi wa serikali. Hata hivyo, malalamiko ya kukatwa au kuenguliwa kwa wagombea wa vyama vya upinzani, hususan kutoka CHADEMA, katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni suala linaloweza kuhatarisha hali ya demokrasia na utulivu wa kisiasa nchini. Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa zaidi ya wagombea 571 kati ya 636 wa CHADEMA waliojaza fomu za kugombea nafasi mbalimbali wameenguliwa hali inayoashiria kuyumba kwa misingi ya haki na usawa wa kidemokrasia Tanzania.
Uamuzi wa kuwaengua wagombea wa upinzani kwa hila si tu ni jambo la kipuuzi, bali pia unaleta wasiwasi kwa wananchi na mashirika ya kimataifa, hasa linapokuja suala la kuaminika kwa tume za uchaguzi na serikali yenyewe. Matukio haya yanasababisha wananchi kupoteza imani yao kwa serikali, viongozi wake, na zaidi sana chama tawala ambacho kinaunda serikali iliyoko madarakani. Kwa ujumla uamuzi huu haukisaidii chama tawala kubaki madarakani, badala yake unachochea chuki, kutoaminika na hasira kwa wananchi.
Pamoja na hilo, uamuzi wa kuwaengua wapinzani unapunguza kwa kiasi kikubwa moyo wa uzalendo wa wapiga kura, na kuwafanya wasione umuhimu wa uwepo wa katiba na sheria za nchi. Wagombea wanaounga mkono vyama vya upinzani wanaweza wasione umuhimu wa kushiriki kwenye chaguzi hizo kwa sababu ya hali ya kutokuwepo kwa uwakilishi wa vyama wanavyoviunga mkono. Hili linaweza kusababisha kutoshiriki kwa wapiga kura na kuzorota kwa michakato ya kidemokrasia.
Kwa wanaounga mkono chama tawala wanaweza wasione kama hili ni janga kwa kudhani itasaidia CCM kushinda kirahisi. Lakini ukweli ni kwamba wananchi wanapovunjika moyo wanaweza kupunguza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo, na au kugoma kujitolea kwenye masuala muhimu ya kitaifa.
Kutoshiriki kikamilifu kwa wananchi kwenye masuala ya kiuchumi na kujitolea kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa nchi. Wawekezaji wa ndani na nje wanaweza kusita kuwekeza kwa kuona nchi inakosa utulivu wa kisiasa unaotokana na upendeleo wa kijinga na ubaguzi dhidi ya vyama vya siasa. Mvutano huo unaweza kwenda mbali zaidi kiasi cha kuathiri sekta za kibiashara na kijamii. Kwa ujumla kitendo cha kubagua au kudhurumu haki ya kundi moja la kisiasa au kijamii ni kuchochea uasi, hasira, kutoelewana, na migawanyiko ya kijamii. Hii inaweza kuathiri mshikamano wa kitaifa na kuhatarisha amani.
2. Mapendekezo kwa Wagombea na Wanachama wa CHADEMA
Wagombea na wanachama wa CHADEMA wanapaswa kutumia vyombo vya sheria kuwasilisha malalamiko yao. Wanapaswa kufungua kesi mahakamani ili kupinga uamuzi wa kuenguliwa kwao na kuhakikisha haki yao ya kugombea inatambuliwa. Katika demokrasia yoyote, njia ya kisheria ni muhimu kwa ajili ya kudai haki. Ingawa katika miaka ya nyuma mahakama na vyombo vingine vvya sheria na dola vilionesha kutoa maamuzi kwa maelekezo kutoka juu, hali hiyo hivi sasa imepungua kwa kiasi fulani kutokana na uwepo wa wanasheria wanaojitambua. Aidha vyama vya siasa vinaweza kuomba msaada wa kisheria toka chama cha wanasheria wa Tanganyika ambacho hivi sasa uongozi wake umejikita katika kulinda na kutetea haki za wote bila hofu.
Pamoja na hilo vyama vya siasa vilivyodhulumiwa haki kwa kuenguliwa wagombea wake vinapaswa kuwaeleza wananchi kwa uwazi mgogoro uliopo kati ya vyama hivyo na tume ya uchaguzi. Vyama vinawajibu wa kufanya kampeni za uhamasishaji na mikutano ya hadhara ili kueleza wananchi hali halisi na kuwahamasisha kutetea demokrasia. Njia hii itawasaidia kupata uungwaji mkono wa jamii na kuhamasisha ushiriki wa wapiga kura.
Sambamba na hilo vyama vya siasa vinapaswa kushirikiana na mashirika ya kiraia na wanaharakati wa haki za binadamu ili kupata uungwaji mkono wa kitaifa na kimataifa. Kwa kufanya kazi na mashirika haya, wanaweza kuongeza sauti zao na kuonesha kuwa wanapigania haki na usawa kwa ajili ya demokrasia ya Tanzania.
Ni vyema pia vyama viimarishe mahusiano yake na vyombo vya dola ikiwa pamoja na majeshi yote ya ulinzi na usalama. Hivi sasa CCM imetengeneza mazingira mazuri ya kuwafanya wapinzani waonekane kama wasaliti wasioitakia mema nchi yao wakati ukweli ni kuwa mfumo wa vyama vingi umeundwa kisheria kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa bahati mbaya sana vyama vya upinzani navyo vimeingia katika mtego huo kiasi cha kutangaza vita na polisi, kuwaita ma CCM na hivyo kujenga uhusiano mbaya na majeshi hayo jambo linalochangia mno vyama hivi kunyanyaswa.
Ni muhimu sana tunapoelekea uchaguzi mkuu wa 2025 vyama vya siasa viimarishe uhusiano wake na majeshi kiasi cha kuanza kupata haki sawa na CCM na hata kupewa upendeleo. Vyama vya siasa visisite kuwaalika viongozi wa vyombo vya dola kwenye mikutano au hafla zao, vitake ushauri wa kiusalama, na ikibidi vyama vijenge tabia ya kuomba ulinzi wa askari polisi wanapokuwa na ugeni au mikutano ya ndani kwa lengo la kujenga ukaribu na maafisa wa polisi katika wilaya au maeneo husika. Sambamba na hilo vyama vya siasa viache tabia ya kutukana maaskari majukwaani kwani kufanya hivyo kuna gharama kubwa kuliko faida. Biblia inaonya kuushinda uovu kwa wema.
3. Mapendekezo kwa Serikali ya Tanzania
Serikali inapaswa kulinda mfumo wa siasa wa vyama vingi nchini ili kujenga demokrasia ya kweli na uchumi thabiti. Viongozi waache kujifikiria binafsi na kulinda maslahi yao na vyama vyao badala yake wajikite katika kulinda maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ustawi wa watu wake. Pamoja na hilo serikali inapaswa kupitia upya sheria na taratibu za uchaguzi ili kuondoa mianya ya ubaguzi wa kisiasa. Kwa kufanya hivyo, serikali itaimarisha uaminifu wa vyama vyote na wananchi kwa ujumla.
Ili kutatua matatizo na malalamiko yaliyojitokeza katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu serikali ianzishe uchunguzi huru kupata ukweli wa malalamiko yanayotolewa na wagombea wa upinzani. Uchunguzi huu utaisaidia serikali kufahamu ukweli na kutoa haki kwa wagombea waliokosewa au kudhulumiwa haki zao. Uchunguzi huru unasaidia kurudisha imani kwa wananchi.
Ili kuondoa malalamiko na kupunguza ubaguzi wa kisiasa ndani ya Tume ya Uchaguzi ni vyema uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi uwe wa uwazi na unaohusisha uwakilishi kutoka vyama vyote vya siasa. Mfumo wa sasa unatoa mwanya kwa watu wa tume kukipendelea chama tawala kwa kila hali. Kuwepo kwa tume huru yenye watu huru kutarejesha imani kwa vyama vyote na wananchi kwa ujumla kuwa Tume haina upendeleo.
Lakini pia serikali inapaswa kuanzisha kampeni za elimu ya uraia ili kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi. Ni muhimu kila raia afahamu kwamba kuwa mwanachama wa chama cha upinzani si uhaini bali ni haki ya kikatiba aliyonayo mtanzania. Kampeni hizi zitawasaidia wananchi kuelewa umuhimu wa ushiriki wa vyama vya siasa katika uchaguzi, zitapunguza migogoro na vita baridi iliyopo kati ya polisi na byama vya upinzani, na kutachochea ushiriki wa watu wenye uwezo mkubwa katika vyama vya siasa.
Hitimisho
Kuwanyima wagombea wa upinzani haki ya kushiriki katika uchaguzi ni kitendo kinachovuruga misingi ya demokrasia, na kinyume cha katiba ya Tanzania. Uamuzi huu unaweza kuwa na athari kubwa kwa utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kijamii, na maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania. Serikali inapaswa kuchukua hatua za kurekebisha na kuimarisha uwazi katika mchakato wa uchaguzi ili kulinda demokrasia. Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani vinapaswa kutumia njia za kisheria na ushirikiano na mashirika ya kiraia ili kupigania haki na usawa. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kulinda demokrasia kwani ni urithi wa taifa kwa vizazi vijavyo.
Rev. Godwin Chilewa
Comments