top of page

Ushindi wa Donald Trump ni Onyo kwa Serikali ya CCM na Funzo kwa Vyama vya Upinzani Tanzania


Ushindi wa Donald Trump dhidi ya Kamala Harris katika uchaguzi wa Marekani wa 2024 unatoa ujumbe muhimu kwa siasa za Tanzania. Funzo kuu linalotokana na ushindi huu ni jinsi mpinzani anayedhaniwa dhaifu anaweza kushinda uchaguzi endapo atatumia mbinu sahihi na kujenga mvuto kwa wapiga kura. Hali hii inafungua njia kwa vyama vya upinzani nchini Tanzania, lakini pia inatoa onyo kwa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania. Vyama vya upinzani nchini Tanzania vinaweza kujifunza mengi ili kujiongezea nafasi ya kufanikiwa, lakini nayo serikali ya CCM inaweza kutumia fursa ya funzo hilo ili kuimarisha nafasi yake ya kubaki madarakani.


(a) VYAMA VYA UPINZANI


Ushindi wa Trump ni funzo na hamasa kwa vyama vya upinzani kuwa uchaguzi unaweza kuwa na matokeo yasiyotarajiwa, na mgombea anayedharauliwa au kupigwa vita kwa nguvu bado anaweza kushinda endapo atatumia mikakati bora. Tena haijalishi serikali iliyoko madarakani ina nguvu kiasi gani, inatumia vyombo vya dola na rasilimali za nchi kiasi gani na au inaungwa mkono na mataifa gani. Kama mgombea wa upinzani na chama chake wakijipanga vyema upo uwezekano wa kuitoa serikali ya chama tawala nadarakani.


Ili kuweza kushinda katika uchaguzi mkuu Tanzania, vyama vya upinzani vinapaswa kwanza kujidhatiti, kuacha siasa legelege na kujenga mtandao imara wa kuwashawishi wananchi kuwaunga mkono. Ni muhimu vyama vya upinzani vioneshe kuwa vinajali maslahi ya watu wa kawaida na siyo tu ya kisiasa. Kujenga taswira ya uzalendo wa kweli na kujitolea kuleta mabadiliko kunaleta hisia za uaminifu miongoni mwa wapiga kura. Ni lazima wapinzani wajenge taswila ya uzalendo, kutetea kweli na kwamba wao ndiyo suluhisho pekee la matatizo ya watanzania.


2. Taswira ya Mpinzani Anayeonewa na Kupigania Maslahi ya Watu wa Kawaida


Trump alitumia tuhuma na mashambulizi dhidi yake kama silaha ya kujenga taswira ya kuwa mpiganaji dhidi ya mfumo uliopo. Vyama vya upinzani Tanzania vinapitia wakati kama aliopitia Trump, kudhibitiwa, kushitakiwa mahakamani, na kuminywa uhuru. Kwa msingi huo vinayo nafasi ya kutumia mikasa hiyo kwa kuwaonesha wapiga kura kuwa upinzani ndio unaojali maslahi ya watu, na kupigania haki za wananchi wanaonyanyaswa na mifumo ya kiserikali. Ni lazima upinzani uwe na ujumbe unaoonesha kuwa wao ni sauti ya watu wa kawaida, wanaopinga utawala wa kibaguzi au wa tabaka tawala. Ikiwa upinzani utaweza kuonekana kama mwakilishi wa watu wa kawaida, una nafasi kubwa ya kuvutia wapiga kura wanaotamani mabadiliko. Bahati nzuri upande wa wapinzani tayari wameshaweka misingi hiyo.


3. Kuwafikia na Kuvutia Wapiga Kura wa Tabaka la Chini na Wenye Kipato cha Kati.


Trump alijipatia uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wapiga kura wa tabaka la chini na la kipato cha kati. Ugumu wa maisha, kuzorota kwa ustaarabu na maadili, na ongezeko la uhalifu kumefanya ujumbe wa Donald Trump kutengeneza mwangwi katika masikio ya watu. Vyama vya upinzani nchini pia vinapaswa kuwekeza kwenye kueneza ujumbe wa matumaini na suluhisho za masuala ya uchumi na ajira, ambazo ni changamoto kubwa kwa tabaka hili. Kwa kuonesha kwamba wanajali masuala ya kiuchumi ya wananchi wa kawaida, uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko kunaweza kuvutia wapiga kura wengi zaidi kutoka maeneo ya vijijini na mijini.


4. Kuongeza Matumizi ya Mitandao ya Kijamii Kama Jukwaa La Kuwafikia Vijana.


Trump alitumia mitandao ya kijamii kufikia wapiga kura wake moja kwa moja, bila kutegemea vyombo vya habari vya kawaida. Mitandao yote kutia ndani X, Facebook, Instagram na Youtube ilifurika matangazo ya kampeni, ujumbe wa Donald Trump na propaganda zenye ushawishi. Vyama vya upinzani nchini Tanzania vinapaswa kuiga mkakati huu wa kutumia mitandao ya kijamii kuwasiliana na wapiga kura, hasa vijana. Hii ni njia ya kueneza ujumbe kwa urahisi, kuvutia kundi kubwa la wapiga kura kwa gharama nafuu, na kuwafikia watu moja kwa moja. Uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi unaweza kuwasaidia kuimarisha kampeni zao na kufikia wapiga kura kwa urahisi. Hata hivyo wapinzani watapaswa kujiandaa na uwezekano wa mitandao hiyo na hata internet kuzimwa waksti wa vuguvugu la uchaguzi.


5. Kuwafikia Wapiga Kura Wote na Kuonyesha Ufahamu wa Changamoto Zao Halisi.


Moja ya udhaifu wa Kamala Harris ulikuwa ni kushindwa kuwafikia wapiga kura wote kwa ujumbe unaoeleweka kwa dhumuni la kuwashawishibkupiga kura. Wakati hoja zake (Kamala) zililenga kwa dhati kukomboa makundi maalum yanayonyanyasika na au kunyimwa haki, wengi wa wanufaika wa makundi hayo hawakuguswa na ujumbe wake na hivyo hawakumpa kura zao

na wengine hawakupiga kura kabisa. Vyama vya upinzani nchini Tanzania vinapaswa kuhakikisha vinawafikia wapiga kura wote kwa njia mbalimbali, wakiwemo wakazi wa vijijini na wa mijini, kuhakikisha watu hao wamejiandikisha kupiga kura, na kuwajengea imani na matumaini kwa chama chao. Hii itasaidia kujenga ujumbe unaogusa masuala ya msingi yanayowagusa wapiga kura na kuwafanya wapate mvuto wa kisiasa.


(b) CHAMA TAWALA - CCM


Kama ilivyo kwa vyama vya upinzani, chama tawala CCM kina mengi zaidi ya kujifunza toka uchaguzi wa Marekani na ushindi wa Trump. Udhaifu wa kampeni ya Harris haukujionesha moja kwa moja kiasi cha kuwafanya wengi waamini angeshinda uchaguzi. Kujiamini kupita kiasi, kumdharau mpinzani wake na kuweka tumaini kwa mashabiki wasiopiga kura na au kigeugeu kumemnyima Harris nafasi ya urais na kukiyoa chama cha Democratic madarakani. CCM inapaswa kujifunza kutodharau wapinzani, kutowanyanyasa na kuamini kwamba itadumu kilele madarakani. Huu ji wakati ambapo CCM inapaswa kujitafakari, kujisafisha, na kuachana na makandokando kwa faida ya chama.


CCM inapaswa kujitangaza kwa vitendo na si kwa maneno kwani ndicho chama tawala. Inapaswa kurejesha matumaini kwa kuondoa rushwa, kuboresha hali ya wananchi, na kuwasilisha ujumbe wa pamoja unaosisitiza mafanikio ya serikali kwa kulinganisha uhuru na ustawi wa watu tangu Rais Samia alipoingia nadarakani na kabla ya hapo. CcM isitegemee kauli inazotoa kwa wananchi kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya maendeleo, uboreshaji wa huduma za afya, na elimu tu. Hayo ni mambo ya msingi lakini yanaweza yasimshawishi mtu kukichagua chama cha mapinduzi. Watu wanataka kusikia mambo yanayowagusa binafsi, hata kama utekelezaji au usimamizi wake ni wa jumla. Watu wanataka kujiona wako salama, wana hakika ya kupata japo milo miwili kwa siku, na hawafumbwi midomo yao wanapoongea. Ni muhimu CCM ioneshe kwamba imedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania kwa vitendo.


2. Kusikiliza Mahitaji na Maoni ya Wapiga Kura


Wapiga kura wanapenda kuhisi wanahusika katika maamuzi. CCM inapaswa kuhakikisha kuwa inapokea maoni ya wapiga kura na kuelezea wazi hatua zinazochukuliwa kuhusu changamoto zinazowakabili. Kujali mahitaji ya wapiga kura na kutoa suluhisho la matatizo yao kutawavutia wapiga kura kuunga mkono chama.


Hivi karibuni viongozi wa CCM wanekuwa wakitoa kauli nyingi zinazoonesha kupuuza maoni ya wananchi, kutojali na kuwa na kiburi cha madaraka. Pengine hili linatokana na viongozi wa CCM kuwa na matumaini ya kupata ushindi katika uchaguzi ujao. Ni muhimu ikumbukwe kuwa wapiga kura ndio wanaoiweka serikali madarakani. Kwa hiyo hata pale wananchi wanapotoa hoja zinazoonekana hazifai au hazina uzito ni muhimu sana viongozi watoe najibu kwa nidhamu na kuonesha kujali badala ya kuonesha dharau na kiburi cha waziwazi.


3. Kuimarisha Umoja na Mshikamano Ndani ya Chama


Hili halizungumzwi sana, wala kutajwa hadharani. Hata hivyo kuna kila dalili kwamba ndani ya chama ya chama kuna mgawanyiko na mivutano inayoweza kudhoofisha nafasi ya ushindi kwa CCM. Mgawanyiko unaweza kuashiria udhaifu na kutoa fursa kwa wapinzani kujinufaisha kisiasa. Kinyume chake umoja wa ndani na mshikamano unatoa picha ya uthabiti na uimara wa chama kwa wapiga kura.  Ni muhimu kwa CCM kuhakikisha kuna mshikamano wa ndani, hasa katika kuunga mkono sera za Rais Samia na ajenda ya maendeleo ya serikali yake.


4. Kuonfoa Matabaka na Kujenga Sera Zinazowagusa Watu wa Tabaka la Kati na La Chini


Ukiwauliza viongozi wa CCM watakwambia chama hicho kimejengwa kwa misingi ya kulinda na kutetea maslahi ya wanyonge. Lakini ukiwauliza wananchi wa kawaida, wanyonge na wapiga kura hali ya chama chao, wengi watakwambia kimetekwa nyara, kimevamiwa na au kina wenyewe. Hayo yote yanaashiria kubadilika kwa mtazamo wa CCM na viongozi wake. Chama kinaelrkea kutekwa na matajiri na watu wenye nguvu na hivyo kuongeza ukuaji wa tabaka kati ya walio nacho na wasio nacho. Ni muhimu sana CCM ijitafakari ikizingatia kuwa wapiga kura wa kipato cha kati na wa vijijini wana ushawishi mkubwa katika uchaguzi. CCM inapaswa kuhakikisha mwenendo wake, viongozi wake, sera na ahadi zake zinazingatia haki, na zinagusa moja kwa moja masuala ya kiuchumi na kijamii yanayohusu kundi hili. Mafanikio ya kiuchumi na kuimarika kwa maisha ya kila siku ya wananchi yataisaidia CCM kujenga uungwaji mkono wa wapiga kura na kuweza kushinda katika chaguzi zijazo.


Hitimisho


Ushindi wa Donald Trump dhidi ya Kamala Harris unatoa funzo muhimu kwa siasa za Tanzania. Kwa vyama vya upinzani, ushindi huu unathibitisha kuwa wanaweza kushinda endapo watajenga taswira ya kuonewa, kutumia vyema mitandao ya kijamii, na kutoa ujumbe unaogusa changamoto za wapiga kura wa kawaida. Kwa upande wa CCM, ni muhimu kuimarisha umoja ndani ya chama, kupambana na rushwa na ubadhirifu kwa nguvu na uwazi, kusikiliza kilio cha wananchi, na kufikisha ujumbe thabiti unaoonesha jinsi chama kinavyoshughulika na masuala ya msingi ya wapiga kura. Kwa ujumla, uchaguzi mkuu ujao Tanzania utategemea sana jinsi vyama vyote vinavyosimamia ujumbe wao na kutekeleza mikakati yao ya kisiasa.

 
 
 

コメント


bottom of page